Wafugaji wengi wamekuwa wakipata ng’ombe
wanaozalisha kidogo na kwa kiwango cha chini kutokana na kuangalia
ukubwa wa gharama ya mbegu wakidhania kuwa ndiyo upatikanaji wa ng’ombe
bora. Vinasaba husaidia kwa kiwango kikubwa katika kupata ng’ombe mzuri
wa maziwa.
Kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa
maziwa hutegemeana na vitu viwili ambavyo ni kuboresha mifugo kwa
kufanya uchaguzi sahihi wa kizazi pamoja na usimamizi mzuri unaojumuisha
lishe kamili, malazi mazuri, upatikanaji wa maji,kuwa karibu na
wanyama pamoja na utoaji wa kinga na tiba dhidi ya magonjwa.
Vinasaba pamoja na usimamizi mzuri ni
vitu viwili vinavyotegemeana. Bila kuwa na uzao mzuri, uzalishaji wa
wanyama pamoja na usimamizi utakuwa wa hali ya chini sana, na bila
usimamizi mzuri wanyama bora hawawezi kuonesha ubora wao katika
uzalishaji.
Uzao mzuri humpa nafasi kubwa mfugaji
kutambua sifa na uzalishaji utakaopatikana katika uzao ujao. Endapo
mfugaji atafanya uchaguzi mbaya basi ni hakika atakuwa na uzalishaji
hafifu wa maziwa, kuzorota kwa afya ya mnyama pamoja na maisha mafupi.
Muda wa kufanya tafiti
Wafugaji wengi wamekuwa wakifikiria
mbegu pale tu ng’ombe anapokuwa tayari anahitaji kupandwa na matokeo
yake ni kuwa, kutokana na haraka ya kutaka kumhudumia ng’ombe huyo, basi
mfugaji atakuwa tayari kuchukua mbegu yoyote ile atakoyopatiwa na
wataalamu. Kwa mantiki hiyo, hakuna muda mfugaji atatumia kuchunguza
aina ya dume aliyetumika kupatikana kwa mbegu hiyo na badala yake,
gharama hutumika kwa kiasi kikubwa kuonesha uwezo wa dume huyo.
Wafugaji wengi hufikiri kuwa kitendo cha
mbegu kuuzwa kwa gharama kubwa ni moja ya njia ya kutambua ubora wa
dume. Wauzaji wengi wamekuwa wakitumia njia hii kuwadanganya na
kuwarubuni wafugaji.
Ni muhimu sana kwa mfugaji anaelenga
kuzalisha maziwa kusoma na kuelewa taarifa zote muhimu zilizotolewa
kuhusu aina ya dume husika. Ili kufanikiwa katika uzalishaji wa maziwa,
ni muhimu kwa mfugaji kuwa makini na kulichukulia kwa uzito suala la
uchaguzi wa dume na kuelewa nini kinahitajika bila kubahatisha. Mfugaji
ni lazima atambue kuwa, dume huchangia asilimia 50 ya kinasaba katika
uzao wake hivyo ni muhimu sana kujua sifa za dume unayemchukua kwa ajili
ya uzalishaji. Pia ubora wa maziwa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na aina
ya dume aliyetumika. Dume wa maziwa hutambulika kwa kuangalia kiwango
cha maziwa yanayozalishwa na ng’ombe aliyepandwa na dume huyo na mtamba
aliyezaliwa na ng’ombe huyo ambapo dume huyo husambaza sifa ya maziwa
kutoka kwa ng’ombe huyo hadi kwa mtamba.
Elewa maelekezo yaliyopo kwenye kabrasha la mbegu
Kielelezo cha vinasaba hutumika kupima
uwezo wa mnyama kusambaza vinasaba vyake kwenda kwa uzao ujao. Katalogi
huwa na taarifa muhimu ambazo zitamsaidia mfugaji kufanya uchaguzi mzuri
wa dume ili kuwa na uhakika wa kuendeleza kizazi baada ya kingine.