Featured

Showing posts with label POULTRY. Show all posts
Showing posts with label POULTRY. Show all posts

UFUGAJI NA UANGALIZI WA KWARE 🐥

*UFUGAJI WA KWARE :*


Sehemu ya Kwanza

Utayarishaji wa banda, Utagaji na uatamiaji mayai, utunzaji vifaranga, uleaji wa vifaranga magonjwa, tiba na kinga.

🔹UTANGULIZI:

Kware ni ndege mdogo mwenye asili ya toka huko Japan. Wakiwa mwituni kware ni ndege wanaohama hama na kuishi mashambani. Rangi ya kware huyu wa mjapan ni yenye madoadoa ya kahawia meupe na meusi yanayoanzia kichwani mwake na hadi mkiani tumboni akiwa na rangi ya kahawia hafi fu. kware pia wanapatikana katika rangi tofauti kama nyeupe tupu, au nyeupe na nyeusi, Kware mkubwa anaweza kuwa na uzito upatao wa gramu 150.

🔹BANDA:

Banda liwe na sifa kama banda la kuku. Kwa kuanza unaweza ukawa na banda la ukubwa wa 1.5m x 1.5m, pia lazima uzingatie usalama
wa vifaranga dhidi ya panya, paka au vicheche. Unatakiwa kuweka ‘magazeti au makasha’ chini kwenye sakafu yatakayosaidia kuondoa hali ya unyevunyevu na pia inakuwa rahisi kulifanyia usafi.

🔹UTAGAJI MAYAI

Wiki ya sita kuelekea ya saba kware wataanza kutaga mayai kila siku. Kwa wastani kware mmoja hutaga mayai 24.

Kware dume humpanda jike kwa muda kidogo, Hapo jike anakuwa tayari kutaga na hutaga mayai 290 hadi 310 kwa mwaka (hii hulingana na lishe nzuri atakayopatiwa).

Mayai ya kware huatamiwa kwa siku 16 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku 2, kuanzia siku ya 16 na hadi 18.Njia bora ya kutotolesha mayai ya kware ni kwa kutumia incubator ambapo mayai huatamiwa kwa wingi ndani ya siku 18.


UTUNZAJI WA VIFARANGA

🔹JUMA LA KWANZA

 Vifaranga wapatiwe chakula “Broiler starter” na maji masafi ya kutosha. Siku ya 1 wawekee ‘GLUCOSE’ kwenye maji, Packet moja kwa lita 6 za maji, na siku ya pili hadi ya tano wape vitamini kama vitalyte kwenye maji, siku ya sita wape vitamini pekee kama Stressvita/Farmvita na siku ya saba wapatie chanjo ya Newcastle.

USAFI: Katika juma hili la kwanza chakula kitawekwa chini na tunashauri kuhakikisha vifaranga hawatelezi na kuathiri miguu.

🔺ZINGATIA: Weka goroli au mawe kwenye manywesheo (drinkers) zako ili kuzuia vifaranga wasizame ndani ya (drinkers) maji na kufa.

🔹JUMA LA PILI: 

Vifaranga wataendelea kupewa chakula Broiler starter na maji safi. Wataendelea kuhitaji ‘mwanga’ wa kutosha muda wote na joto la wastani.

🔹JUMA LA TATU

Uhitaji wa joto utapungua, ila ni kipindi ambacho wanakula chakula zaidi kwa ajili ya kukua. Ni vizuri waendelee kupata taa ili kupata mwangaza utakaowawezesha kula mchana na usiku.

🔹SIKU 21 NA KUENDELEA

KWARE wako hawatahitaji joto tena wawekee taa tu za chemli au energy server kipindi cha usiku, wape chakula na maji ya kutosha zaidi kwa ajili ya kukua.


⚠️ MAGONJWA:

KWARE ni ndege wenye kinga kubwa na ni vigumu sana kushambuliwa na magonjwa kama kuku na mara wanapougua ni rahisi sana kutibika. Magonjwa yanayoweza kuwapata kware ni typhoid, mafua na E.Coli.

🔹TIBA KWA KUTUMIA DAWA ZA DUKANI:

Amprolium kwa ugonjwa wa kuharisha damu/ugoro (Coccidiosis), Fluban, Colirid au Doxycol kutibu mafua (Coryza) na Esb3, au Trimazine, Typhoprim, Ancoban hutumika kwa homa ya matumbo (Typhoid).

🔹TIBA MBADALA

Waweza kuwatibu vifaranga au kware wako kwa kutumia tiba mbadala ambayo pia ni rahisi, gharama nafuu na bora zaidi kuliko kutumia madawa yaliyochanganywa na kemikali na yenye gharama. Vifuatavyo ni vitu vya asili vinavyotumika kutibu magonjwa mbali mbali ya kware na yanayopatikana kwa wingi katika maeneo ya mfugaji. Madawa haya hutumika kwa kiwango cha wastani na hayana kipimo maalum kwani hata ukiyazidisha hayana madhara.

🔹MAJANI YA MWAROBAINI

Madawa haya hutumika kutibu kuharisha damu pamoja na mafua kwa vifaranga vya kware Chukua kiasi kidogo cha mwarubaini kisha twanga vizuri kupata maji maji. Kamua maji yale, kisha weka katika maji uliyoandaa kuwanywesha vifaranga wako. Kata vipande
vidogovidogo vya aloe vera (jani moja laweza kutosha) na tia katika maji yaliyochanganywa na mwarobaini, kisha wapatie vifaranga wanywe (Aloe Vera) itaendelea kujikamua yenyewe ikiwa ndani ya maji huku vifaranga wakiendele kunywa).

🔹KITUNGUU SWAUMU:

Hii hutumika kukinga na kutibu vifaranga vya Kware wanaosumbuliwa na kuharisha damu. Unachukua kitunguu swaumu na kuondoa maganda ya nje kisha kusafi sha na kukata vipande vidogo sana, na kuwawekea kama chakula. Vifaranga wanapenda sana vitunguu hivyo na watakula kwa kasi kama chakula lakini ni tiba tayari. Unaweza kuwapatia kila siku hadi watakapopona.

🔹MAZIWA:

Maziwa yanayotokana na ng’ombe pia hutumika kutibu ugonjwa wa kuhara pamoja na kuwapa nguvu kware waliolegea. Mnyweshe maziwa hayo kware anayeumwa bila kuyachemsha na umnyweshe maziwa ya kutosha kiasi cha kushiba. Unamnywesha mara tatu kwa siku. Hakikisha maziwa unayotumia yanatoka kwa ng’ombe wanaotibiwa kila mara.

⚠️ ANGALIZO:

Siyo lazima kwale waugue ndipo uwapatie tiba hizi. Hakikisha unawapa tiba kabla hata hawajaugua hivyo utawakinga na magonjwa hayo. Waweza kuchanganya madawa hayo yote kwa wakati mmoja kwani hayana madhara.

Endapo madawa ya asili hayapatikani katika eneo la mfugaji basi waweza kuwatibu kwale kwa madawa yafuatayo ambapo vipimo huelezwa moja kwa moja kwa maandishi katika madawa hayo au kuelezwa na muuzaji pale utakaponunulia

🔺CHANJO

Kware wapatiwe chanjo ya “kideri/mdondo” kwa dawa inayoitwa ‘Newcastle’ lasota au T2. Siku ya 7. Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.

Wapewe chanjo ya “gumboro”. inapofi ka Siku ya 14.

Siku ya 21 lazima warudie chanjo ya “Newcastle” na kila baada ya miezi 3 na hakikisha unarudia chanjo ya Newcastle.

UFUGAJI WA FUNZA KIBIASHARA NA JINSI YA KUTENGENEZA FUNZA

funza ni nini? 
Funza hawa ni moja tu kati ya hatua za ukuaji za wadudu walukao, watu wengi hufikili hao funza hubaki kuwa funza mpaka mwisho jambo ambalo si la kweli hawa funza ni larval stage ya ukuaji wa wadudu ambapo wadudu hao wapepelukao hutua na kutaga mayai yao.


Wengine wanachukulia hawa wadudu ni uchafu na kinyaa ila FUNZA ni wadudu wenye PROTINI nyingi ambayo INAHITAJIKA sana kwa UKUAJI wa KUKU,SAMAKI,Nguruwe na mifugo mingine.

Utengenezaji wa Funza ktk kulisha mifugo hupunguza sana gharama za Chakula.

Zipo njia nyingi za Kutengeneza FUNZA.Ila NJIA RAHISI ni;Chukua Kinyesi cha Kuku/ng'ombe jaza kwenye dumu lililokatwa kisha weka pumba za mahindi kwa juu halafu nyunyuzia maji kidogo ili kuwavutia NZI waweze kutaga mayai hapo.Endelea kunyunyizia maji kwa siku 2 zaidi kisha acha.SIKU YA 4 FUNZA WATAANZA KUTOKEA,WAKUSANYE,WAOSHE NA KISHA WAPE KUKU WALE WAFAIDI.

Katika Nchi za wenzetu kuna Viwanda kabisa vya Kutengeneza FUNZA ambao hukaushwa na kuuzwa kwa nchi zingine.

Hii inaweza ikawa FURSA PIA hata Hapa Kwetu TANZANIA.Maana ni Rahisi na Soko lake ni Kubwa SANA.Na Ni kitendo cha Wiki Moja TU,unaanza Kula FAIDA za KUTENGENEZA FUNZA.

KITABU CHA UFUGAJI BORA WA KUKU: UTANGULIZI

UTANGULIZI



Tanzania ni nchi ambayo watu wake ni wafugaji hasa kuku wa kienyeji, ufugaji huu hufanywa hasa na wafugaji wadogo wadogo wahishio maeneo ya vijijini. Ufugaji wa kuku wa kisasa ufanywa hasa na wafugaji wahishio mijini, lakini mahitaji ya Watanzania bado ni makubwa kulingana na idadi (yaani ufugaji wa kuku mjini na vijijinji) na ukilinganisha na ongezeko la watu katika nchi. Vile vile mazao yanayopatikana ni kidogo sana na hafifu.

Kuku wa kienyeji kwa wastani anataga mayai 40 hadi 60 kwa mwaka badala ya mayai 80 hadi 100 kwa mwaka kama atatunzwa vizuri. Hali kadhalika wastani wa uzito wa kuku mmoja ni wa chini sana (kilo 0.75 hadi 1.0) katika umri wa zaidi ya mwaka mmoja: Iwapo atatunzwa kwa kufuata kanuni za utugaji bora ana uwezo wa kufikia uzito wa kilo 1.0 hadi 1.5.

Kuku wa kisasa ana uwezo wa kutaga mayai zaidi ya 250 kwa mwaka na kuwa na uzito wa kilo 1.5 hadi 2 katika umri wa miezi miwili (wiki nane). Uzalishaji mdogo wa kuku hawa unatokana na kutokuwepo kwa utaalamu wa kutosha wa utunzaji wa kuku wa kienyeji. Vile vile matunzo ya kuku wa kisasa hayajafikia kiwango kinachotakiwa.

Ili mfugaji aweze kujipatia mazao mengi na bora ni muhimu azingatie kanuni za ufugaji bora wa kuku. Kanuni hizo ni pamoja na ujenzi wa mabanda bora ya kuku na vifaa vinavyohitajika katika mabanda hayo, uchaguzi wa njia sahihi za ufugaji, jinsi ya kutunza kuku wa kienyeji na wa kisasa. Kanuni zingine ni pamoja na namna ya kutengeneza chakula bora cha kuku, jinsi ya kuzuia magonjwa, utafutaji wa masoko na utayarishaji wa mazao kabla ya kuuza. Maelezo yaliyomo katika kitabu hiki yakizingatiwa yatawawezesha Watanzania kujipatia nyama na mayai mengi ambayo yataongeza ubora wa afya zao na kuinua hali za maisha ya Watanzania kwa kuuza mazao ya ziada.

Ni matumaini yangu kuwa kitabu hiki kitawasaidiwa watu wengi ambao wamekuwa na changamoto ya ufugaji wa kuku kwa muda mrefu. Kama kuna lolote basi msisite kuwasiliana nami kupitia utaratibu wowote kati ya hizo zilizoelekezwa mwishoni mwa kitabu.

GHARAMA ZA KITABU HIKI NI TSH 6000 > NAKALA LAINI (0752438521)

BATA MAJI NA FAIDA ZAKE KATIKA UFUGAJI


Habari Mfugaji unayesoma makala zetu za UFUGAJIMAKINI.. Leo tumekuja na makala hii inayoeleza machache kuhusu ufugaji wa Bata maji au Bata wachafu kama wanavyoitwa na wengi


Bata Hawa wanaitwa Bata maji kutokana na tabia yao ya kucheza na maji kwa muda mwingi. Pia Bata Hawa hawawezi Kula bila kuwa na maji pembeni.


FAIDA ZA UFUGAJI WA BATA MANI (URAHISI WAKE)
  1. Wanakua kwa haraka tofaut na kuku
  2. Utotoaji wake ni mzuri tofauti na kuku kwani mayai ya bata yana uwezo wa kutunza joto kwa muda mrefu
  3. Vifaranga wa Bata hawahitaji joto wakat wa ukuaji wao kwa sababu ya ngozi yao kuwa na manyoya mengi.
  4. Sio wepesi kushambuliwa na magonjwa kama kuku
  5. Hawahitaji uangalizi wa karibu kama kuku
  6. Wanataga mayai makubwa na yenye virutubisho asili( kiini cha njano)
  7. Wana kitoweo(nyama tamu)
  8. Wanafikia uzito mkubwa hadi kilo sita(6) kwa Bata dume
  9. Wanahimili mazingira yote ya joto na baridi.
  10. Soko lake ni la uhakika hasa kwa jamii zinazopenda nyama ya Bata kama vile Upareni
Ufugajimakini tupo kwajili ya kuhakikisha Mfugaji wa Bata anapata soko la uhakika na Yule anayehitaji Bata wa kufuga anapata ili kutimiza malengo ya kila mmoja
KARIBU UFUGAJIMAKINI TUKUHUDUMIE


UFUGAJI WA KUKU WA NYAMA (BROILER). KATIKA ENEO DOGO LISILOZIDI MITA 1. KWA KUKU 100.



*Eneo linalohitajika ni mita mbili (2), Kwa maana ya Urefu wa mita mbili(2) na Upana wa mita moja(1).
Huu ni ufugaji wenye tija kwa wale wafugaji wenye eneo dogo.

*Kinakachofanyika katika hilo eneo ni ujenzi wa ghorofa/shelves tano(5) kwenda juu kwa ajili ya kufugia kuku.
*Urefu unaoshauriwa wa kila shelf/chumba kimoja ni futi moja na nusu hadi mbili.
*Katika kilachumba/shelf unashauriwa kuweka kuku ishirini, kwa maana ya kuku 10 katika eneo la mita 1.
*Ukichukua idadi ya kuku katika kila chumba (20) mara idadi ya vyumba 5, watapatikana kuku mia(100) katika eneo la mita 2.
*Kumbuka kuwa unaweza kufanya mabadiliko mengine kulingana na eneo utakaloweka ghorofa la kuku.

BANDA LA KULELEA VIFARANGA


Ukipenda kujenga nyumba ya vifaranga itafaa ufi kirie yafuatayo:-
a)    Nyumba ya vifaranga iwe karibu na nyumba yako mwenyewe ili uweze kuwakagua vifaranga wako mara kwa mara.
b)   Ijengwe hatua 20 au zaidi mbali na nyumba ya kuku wakubwa, hii ni kinga mojawapo ya kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa.
c)     Nyumba ya vifaranga isiruhusu ubaridi au unyevu au wanyama waharibifu kuingia. Lakini nyumba iingize hewa na mwanga wa kutosha kila wakati.
d)    Nyumba iwe na eneo la kutosha ili vifaranga wapate nafasi ya kutembea kutafuta chakula na maji bila kubanana.
e)     Ijengwe kwenye sehemu isiyoelekea upepo unaotoka kwenye nyumba ya kuku wakubwa. Tahadhari hii husaidia vifaranga kuepukana na magonjwa yanayoenezwa na upepo.


Eneo: Vifaranga hawahitaji eneo kubwa katika muda wa majuma 4 ya kwanza. Nafasi inayohitajiwa kwa kukadiria ni meta za eneo 1 kwa kila vifaranga 16. Kwa mfano nyumba yenye Meta 10 za mraba inatosha kulea vifaranga 160 hadi umri wa majuma 4. Vipimo vya nyumba yenye eneo kama hili inaweza kuwa na hatua 5 kwa hatua 4 au hatua 3 kwa 3.25. Utajenga kutegemea na eneo ulilonalo. Baada ya majuma 4 ya umri ongeza nafasi na uwape vifaranga eneo la kuwatosha.

Sakafu: Sakafu nzuri katika nyumba ya vifaranga ikiwezekana inafaa ijengwe na simenti iliochanganywa na zege. Ili kupunguza gharama, unaweza kutumia vifaa vya ujenzi vinavyopatikana kirahisi katika eneo lako vitumikavyo kusiriba sakafu kama udongo wa kichuguu au unaweza kulainisha kinyesi cha ng’ombe kwa maji na kusiriba eneo lote la sakafu.

Ukuta: Ingefaa kuta za nyumba za kulea vifaranga za matofali, udongo, mabati au debe. Kuta za matofari na udongo zipigwe lipu ili kurahisisha usafishaji wa nyumba au umwagiaji wa dawa. Urefu wa kuta uwe tangu meta 1.8 – 2.4 (futi 6-8). Sehemu ya kutoka chini ya meta 0.9 – 1.2 (futi 3 – 4) izibwe na ukuta wa tofali au udongo na sehemu ya juu iliyobakia yenye meta 0.9 – 1.2 (futi) 3-4) ijengwe kwa wavu wa chuma au fito.

Mbao: Nguzo za miti au mbao zilowekwe dawa ya mbao kama vile “Dudu killer” au oili chafu ili kuzuia kuoza. Ukitumia miti ni vizuri uondoe magome ambayo yanaweza kuweka vimelea na wadudu.

Madirisha: Unaweza kutumia maboksi, mikeka ya magunia, mapazia ya magunia ni rahisi na yanaweza kuwekwa kwa kupigiliwa misumari kwenye dari na upande wa chini pazia ipigiliwe misumari kwenye ubao ili ininginie.Unaweza kukunja mapazia/magunia ili uingize hewa na mwanga wa kutosha katika nyumba ya vifaranga.

Paa: Mjengo wa paa uwe unaoweza kuwapatia vifaranga hewa ya kutosha hivyo paa liwe na tundu la kutoa nje hewa yenye joto. Kwa kadri utakavyoweza, unaweza kutumia madebe, mabati, makuti au nyasi n.k. kuezeka nyumba ya vifaranga. Sehemu ya paa ikianza kuvuja iezekwe bila kuchelewa.

NJIA BORA ZA UTUNZAJI WA MAYAI YA KUKU

Kwa kawaida kuku huanza kutetea(Kutoa mlio wa ishara ya kutaga) anapofikisha miezi sita hadi minane. Hivyo ni vyema viota viandaliwe mapema wakiwa na umri wa miezi mitano. Kuku anapoanza kutaga akifikisha mayai matatu mfugaji anashauriwa kuondoa kila yai linalozidi hayo matatu kila siku linapotagwa na kuliweka alama ya tarehe au namba kwa kutumia penseli ili kumfanya kuku aendelee kutaga kwa lengo la kufikisha mayai 15 mpaka 20. Mayai yanayoondolewa yawekwe kwenye chombo kikavu kinachopitisha hewa ni vizuri pia kuweka mchanga ndani ya chombo hicho.

Hakikisha ya fuatayo.
Sehemu iliyochongoka iwe chini na pana iwe juu.
Hifadhi sehemu yenye hewa ya kutosha na isiyohifadhi joto
Mayai yasikae kwenye hifadhi hiyo zaidi ya wiki mbili toka siku ya kuanza kutagwa.

UATAMIAJI WA MAYAI NA UANGUAJI WA VIFARANGA
Uatamiaji na uanguaji wa kubuni - Mfumo huu hutumia mashine za kutotoleshea vifaranga (Incubators) hutumika kuangua mayai mengi kati ya 50 hadi 500 kwa wakati mmoja Mashine zinazotumika kutotoleshea vifaranga wa kisasa zinaweza kutumika pia kutotoleshea wa kienyeji.
Uatamiaji na uanguaji wa asili

KUCHAGUA MAYAI YA KUANGUA.
Hili nalo ni muhimu kuzingatia. Ni vizuri kuchagua mayai ya kuatamia ili mayai yasiyofaa yaweze kuuzwa au kutumiwa nyumbani kwa chakula. Mayai ya kuatamia yawe na sifa zifuatazo
Yasiwe na uchafu yawe masafi
Yasiwe na nyufa
Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo
Yasiwe madogo wala makubwa bali yawe na ukubwa wa wastani kulingana na umbile la kuku.
Yasiwe mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha kali sana.
Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili toka yalipotagwa
Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye joto.

KUMTAYARISHA KUKU WA KUATAMIA
Pamoja na matayarisho hayo zingatia kumuwekea mayai yasiyozidi 15 pia ni vizuri yasipungue 12. Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri n.k. Kuwepo kwa wadudu hao huwafanya kuku wakose raha na kutotulia kwenye viota vyao. Hali hii husababisha kuanguliwa kwa Vifaranga wachache.
Sasa unatakiwa kufanya yafuatayo:-
Nyunyiza dawa ya kuua wadudu ndani ya kiota
Pia mnyunyuzie dawa kuku anayetarajia kuatamia
Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa jivu ili kuepuka kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.

Ni vizuri kuifanya kazi hii ya kumuandaa kuku anayetaka kuatamia wakati wa usiku. Pia ifahamike kuwa kwa kawaida kuku huatamia mayai yake siku 21.

PIA JIFUNZE MBINU ZA KUATAMIA MAYAI MENGI KWA NJIA ZA ASILI.
Iwapo una kuku wengi wanaotaga kwa wakati mmoja ni vema ukawafanya wakaatamia na kutotoa pamoja.
Unachotakiwa kufanya ni kuchagua mayai ya kuatamia ukianzia na yai la mwisho kutaga.
Unaweza kuwaandaa kuku wako zaidi ya mmoja ili waanze kuatamia kwa pamoja na kupata vifaranga vingi kwa mara moja kuku wa kwanza anapoanza kuatamia. Mwekee mayai viza au ya kuku wa kisasa kwani kuku huatamia hadi mayai yanapoanguliwa hivyo ukimuwekea mayai yasiyo na mbegu atakaa hapo muda mrefu hadi vifaranga watoke.

UTEKELEZAJI WAKE.
Kuku anapotaga kila siku weka alama ya namba au tarehe kulinganisha na siku anayotaga
Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee mayai viza au ya kisasa huku ukiendelea kuweka alama mayai yanayotagwa kila siku.
Mara kuku anapoanza kuatamia muongezee mayai ya uongo yafikie 8 hadi 10
Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi utakapoweza kupata idadi itakayoweza kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja.
Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa kuondoa mayai ya uongo na kuwawekea mayai ya ukweli wakati wa usiku.

MUHIMU.
Mayai ya kuatamia yasishikwe kwa mkono ulio wazi na wala yasipate harufu za mafuta ya taa, manukato n.k.

JIFUNZE PIA KUTAMBUA MAYAI YALIYO NA MBEGU NA YALE YASUYO NA MBEGU.
Mfugaji anaweza kutambua mayai yaliyo na mbegu na yale yasiyo na mbegu siku ya saba baada ya kuanza kuatamia iwapo atapima mayai kwa kutumia box lililotengenezwa maalum pamoja na tochi yenye mwanga mkali ndani ya chumba chenye kiza. Hii itamuwezesha mfugaji ayatumie mayai yasiyo na mbegu kwa chakula cha familia au kuyauza.

MIFUMO MBALIMBALI YA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI.

Kama nilivoeleza kwenye makalaa iliyopita ya http://ufugajimakini.blogspot.com/2016/07/njia-tofauti-za-kufuga-kuku-faida-zake_5.html zipo njia(mifumo) tofauti za ufugaji wa kuku hawa
A. MFUMO HURIA
Katika mfumo huu kuku huachiwa wakitembea toka asubuhi wakijitafutia chakula na maji na kufungiwa kwenye vibanda visivyo rasmi wakati wa usiku. Huu ni mfumo rahisi lakini si nzuri kwa mfugaji wa kuku wengi kwani atahitaji eneo kubwa la ardhi.

FAIDA. 
Mfumo huu una faida za gharama ndogo za uendeshaji kiujumla.

HASARA
Uwezekano mkubwa wa kuku kuliwa na vicheche, kuibiwa mitaani n.k
Kuku huweza kutaga popote na kusababisha upotevu mkubwa wa mayai.
Ni rahisi kuku kuambukizwa magonjwa
Utagaji unakuwa si nzuri kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Uwekaji kumbukumbu si nzuri.
Ni vigumu kugundua kuku wagonjwa hivyo kusababisha ugumu katika utoaji wa tiba.

UTUMIAJI NZURI WA MFUMO HUU
Kuku wajengewe banda kwa ajili ya kulala nyakati za usiku na liwasaidie wakati mwingine wowote hali ya hewa inapokuwa si nzuri.
Kuku wapatiwe chakula cha ziada na maji.
Kuku waandaliwe kwa viota vya kutagia.
Kuku 100 ni vizuri wakitumia eneo la ardhi la ekari 1.
B.MFUMO NUSU HURIA
Huu ni mfumo ambao kuku hujengewa banda rasmi na banda hilo huzungushiwa uzio/ wigo. Mfumo huu ni ghari kiasi ukilinganisha na mfumo huria lakini huweza kumpatia mfugaji faida haraka sana.

FAIDA
Sehemu ndogo ya kufugia hutumika kuliko ufugaji huria, utunzaji wa kuku ni rahisi ukilinganisha na mfumo huria, Ni rahisi kutibu magonjwa ya mlipuka kama mdondo (Newcastle desease), Upotevu wa kuku na mayai ni mdogo sana ukilinganisha na mfumo huria.
C. MFUMO WA NDANI
Kuku hujengewa banda rasmi na hufugwa wakiwa ndani. Mfumo huu kuku huwekwa kwenye mabanda ambayo sakafu hufunikwa kwa matandiko ya makapi ya mpunga, takataka za mbao(randa), maganda ya karanga au majani makavu yaliyokatwa katwa.

FAIDA
Mfumo huu unahitaji eneo dogo la kufugia, uangalizi mzuri na rahisi wa kuku, Joto litokanalo na matandiko lina uwezo wa kuua vimelea vya maradhi, kuku wanakingwa na hali ya hewa mbaya na maadui wengine.

HASARA
Uwezekano wa kuku kudonoana ni mkubw na pia Gharama za ujenzi wa mabanda

UTUMIAJI MZURI WA MFUMO HUU.
1. Matandiko yageuzwe kila siku
2. Kila mara matandiko yawe makavu kwa kuwa na madirisha yanayopitisha hewa ya kutosha, ambayo yatatoa unyevunyevu hewa chafu ikiwemo ammonia.
4. Mita mraba moja hutosha kuku 5 hadi 8.

Mtaji wa kufuga kuku wa kienyeji, mchanganuo wake na namna ya kupata soko

Mchanganuo


Pengine umekuwa ukiwaza sana nini ufanye ili uweze kufanikiwa na kuondokana na adha za umaskini. Yako mambo mengi ya kufanya mimi nataka kukufungua macho kwa jambo moja tu tena kwa uchache. Jambo hili anaweza kulifanya mwenye mtaji mkubwa au mdogo.
Somo langu ni dogo lakini naamini wapo watakaopata mafanikio makubwa sana. Sasa kuwa makini zaidi. 

Unaweza kuanza kwa mtaji wa Mil.1 mpaka laki tano au hata chini ya hapo.

Mfano. Unaweza kutumia Tsh 250,000 kununua kuku 25 kwa bei ya Tsh 10,000 kwa kuku mmoja (kadirio la juu) Majogoo watakuwa 5 kwa uwiano wa 1:4. 

Hii ina maana kuwa wakishaanza kutaga utakuwa na

vifaranga 20 x 10 = 200 Watunze vizuri.

Wale vifaranga tunakadiria kuwa makoo(majike) watakuwa 150 ambao ndani ya miezi 3 au zaidi nao wataanza kutaga.

Utakuwa na kuku 200 + 25 =225 ndani ya miezi 6. Miezi 6 inayofuata 225 - (majogoo 55) = 170 Hii ina maana kuwa 170 x 10= 1,700. 

Ndugu mfuatiliaji, hayo niliyotoa ni makadirio ya chini sana hivyo mpaka mwisho wa mwaka utakuwa na kuku zaidi ya 2000. Mwaka utakaofuata utakuwa na kuku wangapi baada ya kuuza kuku 1,000. Miaka 2. 750(majike) x 10 = 7500 (uza wengine) 3000 x 10 = 30,000. Kutegemea na uwezo wako mpaka mwisho wa mwaka wa pili utakuwa umefanikiwa sana.

Kumbuka huu ni mwongozo tu, fanya utafiti na ufuatilie zaidi.

NB. Kumbuka kuku ninao wazungumzia hapa ni wale wa kawaida wa kienyeji.Fuatilia zaidi kuhusu matibabu na matunzo mengineyo.

UTANGULIZI
Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kwa namna moja au nyingine kutoa mchango wangu kwa mtindo huu. Huu ni kama mwongozo tu wa nini utakabiliana nacho au unatakiwa kufanya katika zoezi zima la ufugaji wa kuku wa kienyeji. Nimeamua kuuleta kwenu ili kwa mtu mwenye malengo ya kufanikiwa kupitia ufugaji wa kuku ajue mlolongo mzima na changamoto ambazo atakabiliana nazo.

A.KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?
1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya kuku kama mdondo, ndui ya kuku n.k ili kuweza kuwaendeleza.
2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.
3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA KUKU WA KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)
5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.

B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.
Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza zile ambazo kwa wengine huenda zikawa ni ngeni kwao.
- Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata maelezo jinsi yai la kuku wa kienyeji linavyoweza kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba mbadala)
- Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
- Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu na chanjo ya ndui mara mbili kwa mwaka
Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza
Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
Kula mayai na kuku kadri uzalishaji unavyoongezeka.
Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili ya uendelezaji wa kuku

C:MAPUNGUFU
Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.


D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI
Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Hata hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka. Baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:

a. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.

Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.
(i)          KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama mgongo ukiwa wima. Wana manyoya machache mwilini na hasa kifuani, vilemba vyao ni vidogo. Majogoo huwa na wastani wa uzito wa Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana uzito wa wastani wa gm 45. Kuku hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Zanzibar.


(ii) CHING'WEKWE

Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa mtu asiyekuwa na meno kulitamka wana sifa zifuatazo.
Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm 37. Kuku hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi maeneo ya CHAKWALE mkoani Morogoro na pia sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai mengi sana kuliko aina nyingine ya kuku wa kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa sana kwa biashara ya mayai.


(iii)UMBO LA KATI

Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9, Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio hasa wanaoitwa wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti. Utafiti umeonyesha kuwa kuku hawa hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo (Castle desease) 
Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka kwenye aina hii ya kuku na kutoa matunzo mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika anaweza kupata kuku walio bora na wenye uzito wa kutosha pia kutaga mayai mengi na makubwa.


(iv) SINGAMAGAZI

Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa wana utambulisho maalum kutokana na rangi zao. Majogoo huwa na rangi ya moto na mitetea huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito wa wastani wa kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2 mayai gramu 56.

(v) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya. Asili hasa ya kuku hawa ni kutoka nchi ya jirani ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana damu ya kuku wa Kizungu "Black Australop". Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49

(vi) PEMBA 
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea Kg 1 mayai wastani gm 42

(vii) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6, mitetea kg 1.2 mayai gm 42. Kuku hawa wa Unguja na Pemba wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa ni wadogo.