Aina mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo
kiwango cha maandalizi yako ni muhimu sana. Unahitajika kufahamu kuwa,
unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji
ya awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala
hili limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa
hujiingiza katika shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi
yanayotakiwa pamoja na kuweka mipango thabiti.
Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na ya kuvutia ambayo huwa na
faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa yule anayependa
kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara hata
kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya kufuga.
Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya jambo muhimu sana ambalo
likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe wa maziwa kuwa na
uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji.
ng’ombe wa maziwa bora zaidi kufuga kwa lengo la kuzalisha ni hawa hapa
Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili
ya lishe na mambo mengine yako sawa, ng’ombe wa maziwa ni lazima
kuzalisha kulingana na umbile lake na uwezo wake kamili. Kama utaweza
kumudu kufuga ng’ombe halisi wa maziwa, ni lazima pia utambue kuwa
uzalishaji wa juu wa maziwa uhitaji pia usimamizi wa hali ya juu. Kwa
maana hiyo, ni vyema kufuga ng’ombe wa kiwango cha kawaida (ikiwezekana
chotara) ambaye ataendana na uwezo wako wa kumtunza.
Ni vyema tukaangalia aina mbili za ng’ombe wa maziwa ambao wana uwezo wa kuzalisha maziwa mengi;
(i) Freshiani (Friesian)
Ng’ombe aina ya freshiani ni rahisi
kumtambua kutokana na kuwa na rangi nyeusi na nyeupe, na ni ng’ombe
wenye uzalishaji bora wa maziwa. Wanyama hawa ni wakubwa na pia wanaweza
kuwa na mabaka meupe na meusi au mekundu na meupe. Ikiwa watalishwa
vizuri, freshian aliyefikia umri wa kukomaa huwa na uzito wa hadi
kilogramu 550 na urefu wa sentimeta 150 kutoka begani. Mtamba huweza
kupandwa, akiwa na umri wa miezi mitano huku akiwa na uzito wa kilogramu
360.
Wakati baadhi ya ng’ombe wakiwa na uwezo
wa kuishi kwa muda mrefu, uwezo wa kawaida wa kuishi kwa Freshiani ni
miaka sita. Hata hivyo, aina hii ya ng’ombe ni wazalishaji wazuri wa
maziwa ambao huweza kuzalisha kilogramu 7800 kwa wastani kwa muda wa
siku 360 yakiwa na kiwango cha chini cha mafuta ikilinganishwa na aina
nyingine ya ng’ombe.
Aidha, aina hii ya ng’ombe huhitaji
ulishaji mkubwa hivyo hushauriwa kwa wafugaji wenye uhakika wa kuwa na
lishe bora na ya kutosha kwa mwaka mzima.
(ii) Ayrshire
Aina hii ng’ombe huwa na miraba ya kahawia na nyeupe karibu sawa na aina nyingine ya ng’ombe ambao huelekea kuwa na rangi ya (Mahogany).
Ng’ombe hawa huwa na wastani wa kawaida, na uzito wa kilogramu 540
katika umri wa ukomavu. Aidha, humudu aina yeyote ya ufugaji na si
rahisi kupata matatizo yeyote ya miguu.
Ayrshire huweza kufanya vizuri
katika malisho ya aina yeyote tofauti na aina nyingine ya ng’ombe wa
maziwa. Kukiwa na usimamizi mzuri na ulishaji mzuri, wastani wa
uzalishaji wa maziwa ni kilogramu 5400 ikiwa na kiwango cha juu cha
mafuta ukilinganisha na Freshian. Aryshire ni aina nzuri kwa kufuga hasa
kutokana na nguvu aliyonayo pamoja na uzalishaji mkubwa wa maziwa.
Ng’ombe wa aina hii, hutambulika kwa kuwa na umbo zuri pamoja na chuchu
zake kuonekana kuwa zenye ubora. Aidha, utungaji wa maziwa yake,
umefanya maziwa yake kuonekana ni mazuri sana katika uzalishaji wa siagi
na jibini.
Maziwa ya Ayrshire yanafahamika
kama “maziwa bora ya kunywa” kutokana na uwezo wake wa kuwa na mafuta ya
kutosha na kiasi kikubwa cha protini. Kwa mfugaji anayeanza, aina hii
ya ng’ombe ni nzuri sana kuanza nayo kasha baadaye kuongeza freshiani
baada ya uwezo wako wa kuhudumia kuwa imara. Mifugo ya asili ni ghali
sana na ni ngumu pia kuwapata, hivyo basi, njia rahisi kwa wafugaji wa
maziwa wanaoanza ni kutafuta ng’ombe bora wa kawaida ambao mara nyingi
huwa ni chotara, kisha kuwaboresha kwa kutumia mbinu ya kupandikiza dume
bora na mwenye uzalishaji mkubwa. Na hii huhitaji elimu ya kutosha
kuhusu uchaguzi wa madume.
*Muhimu: Wakati wa kununua
ng’ombe kwa ajili ya kufuga, ni vyema mfugaji ukatambua kuwa,
wazalishaji wa maziwa mara nyingi hawauzi ng’ombe wao wenye uzalishaji
mzuri, badala yake huuza wale ambao hawazalishi kwa kiwango kizuri, wale
wenye matatizo kama kutokushika mimba, wenye matatizo ya joto na wale
ambao hushambuliwa na magonjwa mara kwa mara. Kwa maana hiyo, pamoja na
aina ya ng’ombe unayehitaji kununua, ni muhimu sana kuwa mwangalifu
usije ukanunua ng’ombe mwenye shida yoyote kwani hapo ndipo mwanzo wa
uzalishaji wako kuja kuwa wa matatizo na kutokufikia lengo.
2 comments
Write commentsNashukuru kwa elimu yako, nami ninatarajia kuanza ufugaji na biadhara hiyo ya ng'ombe wa maziwa. Je, ni wapi naweza kupata mbegu bora na kwa bei gani?
ReplyElimu nzuri sana
Reply