Featured

Dume Mzuri Kwa Uzalishaji Wa Ng’ombe Wa Maziwa

http://ufugajimakini.blogspot.com/
Tunaangalia uchaguzi wa dume mzuri kwa uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa, pamoja na aina ya malisho ambayo mfugaji anaweza kuyatumia kuweza kukabiliana na changamoto ya malisho kwa ng’ombe.
Wafugaji wengi wamekuwa wakipata ng’ombe wanaozalisha kidogo na kwa kiwango cha chini kutokana na kuangalia ukubwa wa gharama ya mbegu wakidhania kuwa ndiyo upatikanaji wa ng’ombe bora. Vinasaba husaidia kwa kiwango kikubwa katika kupata ng’ombe mzuri wa maziwa.


http://ufugajimakini.blogspot.com/
Kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa maziwa hutegemeana na vitu viwili ambavyo ni kuboresha mifugo kwa kufanya uchaguzi sahihi wa kizazi pamoja na usimamizi mzuri unaojumuisha lishe kamili, malazi mazuri, upatikanaji wa maji,kuwa karibu na wanyama pamoja na utoaji wa kinga na tiba dhidi ya magonjwa.


Vinasaba pamoja na usimamizi mzuri ni vitu viwili vinavyotegemeana. Bila kuwa na uzao mzuri, uzalishaji wa wanyama pamoja na usimamizi utakuwa wa hali ya chini sana, na bila usimamizi mzuri wanyama bora hawawezi kuonesha ubora wao katika uzalishaji.


Uzao mzuri humpa nafasi kubwa mfugaji kutambua sifa na uzalishaji utakaopatikana katika uzao ujao. Endapo mfugaji atafanya uchaguzi mbaya basi ni hakika atakuwa na uzalishaji hafifu wa maziwa, kuzorota kwa afya ya mnyama pamoja na maisha mafupi.


Muda wa kufanya tafiti


Wafugaji wengi wamekuwa wakifikiria mbegu pale tu ng’ombe anapokuwa tayari anahitaji kupandwa na matokeo yake ni kuwa, kutokana na haraka ya kutaka kumhudumia ng’ombe huyo, basi mfugaji atakuwa tayari kuchukua mbegu yoyote ile atakoyopatiwa na wataalamu. Kwa mantiki hiyo, hakuna muda mfugaji atatumia kuchunguza aina ya dume aliyetumika kupatikana kwa mbegu hiyo na badala yake, gharama hutumika kwa kiasi kikubwa kuonesha uwezo wa dume huyo.


Wafugaji wengi hufikiri kuwa kitendo cha mbegu kuuzwa kwa gharama kubwa ni moja ya njia ya kutambua ubora wa dume. Wauzaji wengi wamekuwa wakitumia njia hii kuwadanganya na kuwarubuni wafugaji.


Ni muhimu sana kwa mfugaji anaelenga kuzalisha maziwa kusoma na kuelewa taarifa zote muhimu zilizotolewa kuhusu aina ya dume husika. Ili kufanikiwa katika uzalishaji wa maziwa, ni muhimu kwa mfugaji kuwa makini na kulichukulia kwa uzito suala la uchaguzi wa dume na kuelewa nini kinahitajika bila kubahatisha. Mfugaji ni lazima atambue kuwa, dume huchangia asilimia 50 ya kinasaba katika uzao wake hivyo ni muhimu sana kujua sifa za dume unayemchukua kwa ajili ya uzalishaji. Pia ubora wa maziwa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya dume aliyetumika. Dume wa maziwa hutambulika kwa kuangalia kiwango cha maziwa yanayozalishwa na ng’ombe aliyepandwa na dume huyo na mtamba aliyezaliwa na ng’ombe huyo ambapo dume huyo husambaza sifa ya maziwa kutoka kwa ng’ombe huyo hadi kwa mtamba.


Elewa maelekezo yaliyopo kwenye kabrasha la mbegu


Kielelezo cha vinasaba hutumika kupima uwezo wa mnyama kusambaza vinasaba vyake kwenda kwa uzao ujao. Katalogi huwa na taarifa muhimu ambazo zitamsaidia mfugaji kufanya uchaguzi mzuri wa dume ili kuwa na uhakika wa kuendeleza kizazi baada ya kingine.

Subscribe to this Blog via Email :